Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (as)- ABNA-, Sheikh Musavi Muqaddam aliyasema hayo katika Mkutano wa Msimu wa Makamu na Wakurugenzi wa Taasisi ya Mashujaa na Masuala ya Wapiganaji wa Kiislamu, ambapo alisisitiza umuhimu wa kutumia muda ipasavyo na kusimamia wakati vizuri, kama inavyoelekezwa katika mafundisho ya Kiislamu.
Alisema:
“Ikiwa muda utapotea hauwezi kurudi tena, na muda una nafasi muhimu katika matukio yanayoendelea duniani leo. Hatupaswi kuupoteza muda, bali tuwe na ufuatiliaji wa mambo na kuwa na utambuzi wa wakati sahihi wa kuchukua hatua, kwani karne ya 21 ni zama ambazo msingi wake ni umuhimu wa muda.”
Akizungumzia hali ya dunia na migogoro ya kivita katika eneo la Mashariki ya Kati, alisema:
“Dunia haipaswi kujengwa juu ya uongo. Ikiwa jamii itafuata uongo, matokeo yake yatakuwa mabaya, kama tunavyoshuhudia leo pale ambapo utetezi wa haki za wanyonge haujafikia popote.”
Sheikh Musavi Muqaddam aliongeza kuwa:
“Tuna malengo makubwa na kwa ajili ya kuyafikia tutaendelea kupambana. Vita dhidi ya ubeberu tutaendeleza hadi bendera ya haki itakapopepea na thamani za kibinadamu zitaendelea kulindwa. Hatimaye haki itashinda batili, na hilo ndilo hatima ya mwanadamu wote.”
Akinukuu maelezo ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, katika maadhimisho ya siku ya arobaini ya mashahidi wa ‘Uwezo na Heshima’, alisema:
“Kiongozi wa Mapinduzi amesisitiza juu ya kulinda umoja na mshikamano wa kitaifa, pamoja na kuendeleza maendeleo ya kielimu kupitia vipaji na wanasayansi wa taifa.”
Mwisho, Sheikh Musavi Muqaddam aliwasihi viongozi na watumishi wa Taasisi hiyo kuepuka matumizi mabaya na anasa, huku akisisitiza juu ya kuimarisha imani na maadili ya kidini miongoni mwa wafanyakazi.
Alibainisha:
“Kazi lazima ifanywe kwa nia safi na kwa imani ya kweli. Kadiri unavyokuwa na ikhlasi (uaminifu wa moyo), ndivyo baraka na tija ya kazi zinavyoongezeka.”
Your Comment